Tuesday, January 3, 2012

SALAMU ZA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA BENJAMIN WILLIAM MKAPA, KWENYE MAZIKO YA ALIYEKUWA MAKAMU


SALAMU ZA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA BENJAMIN WILLIAM MKAPA, KWENYE MAZIKO YA ALIYEKUWA MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA DR. OMAR ALI JUMA, WAWI, PEMBA, 6 JULAI 2001





Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,
Mheshimiwa Amani Abedi Karume;

Waziri Mkuu,
Mheshimiwa Frederick T. Sumaye;

Waheshimiwa Maspika Wetu;

Waheshimiwa Majaji Wakuu;

Mheshimiwa Waziri Kiongozi;

Mpendwa Mama Salma Omar na Familia ya Marehemu;

Waheshimiwa Mawaziri, Wabunge na Wawakilishi;

Waheshimiwa Viongozi wa Serikali;

Waheshimiwa Viongozi wa Siasa;

Waheshimiwa Viongozi wa Dini;

Ndugu Wananchi;

Mabibi na Mabwana.



Ninaamini wengi wetu ni wacha Mungu, kila mmoja kwa imani yake. Lakini sote tunaunganishwa katika imani zetu na tahadhari tunayopewa siku zote kuwa maisha ya mwanadamu ni mafupi, ni kama maua. Huchanua, na kisha kunyauka. Na hatujui siku wala saa ya kuondoka duniani, na kutangulia mbele ya haki. Ndio maana siku zote Ndugu Zetu Waumini wakiagana na kupeana miadi, hupenda kumaliza kwa kusema, "Inshallah!" Mungu Akipenda!

Na hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Ndugu yetu mpendwa, na kiongozi mwenzetu hodari, mpole na mpenda watu, Makamu wa Rais, Dr. Omar Ali Juma, tunayemzika leo hii kwa majonzi makubwa.

Alikuja dunia miaka 60 iliyopita, akasoma vizuri, na akasomesha wengine; akajenga familia aliyoipenda sana, nayo ikampenda sana; akachanua katika utendaji wake wa kazi hadi kuwa Makamu wa Rais. Na juzi, bila kutarajia, na bila hata kutuaga, ua la maisha yake lililokuwa limechanua likajifumba. Nilikuwa naye hadi saa chache kabla ya mauti kumfikia. Tulizungumza sana, na kucheka sana. Najua, kama ilivyokuwa kawaida yake, alikuwa amejipangia shughuli nyingi za kufanya kesho yake na siku za mbele katika kulitumikia Taifa. Lakini Mwenyenzi Mungu hakupenda iwe hivyo, alipenda amchukue siku ile. Sababu yake hatuijui na wala si kazi yetu kumuuliza. Mapenzi yake yalikuwa tofauti na yetu.

Marehemu ametuachia sisi sote – Familia, Serikali, Chama cha Mapinduzi na Watanzania wote – majonzi makubwa na mshtuko ambao itachukua muda mrefu sana kuuzoea na kuukubali kama jambo ambalo limetokea; hatukuweza na tusingeweza kulizuia.

Na kama ilivyo siku zote, njia bora ya kuonyesha mapenzi yetu na heshima yetu kwa marehemu wetu ni kudumisha na kuendeleza yale aliyoyasimamia na kuyapenda yeye wakati wa uhai wake.

Dr. Omar Ali Juma alikuwa mpenda watu, watu wote, wa dini zote, kabila zote, rangi zote, jinsia zote, na mwelekeo wa kisiasa wowote ule. Hakujua kumnunia au kumchukia mtu kwa sababu ya tofauti kama hizo. Badala yake, alikuwa mcheshi, kiasi ambapo hata pale penye mashaka na kutoaminiana, kicheko kilitawala, kikarejesha utu wetu.

Watanzania wote tumkumbuke na kumuenzi kwa kufuata mwelekeo wake huo. Tupendane wote, na kuheshimiana sote, maana wote sisi ni ndugu wamoja, wana wa Taifa la Tanzania. Na hata pale tukitofautiana, bado tunaweza kutaniana, tukacheka, tukashirikiana kujenga nchi, na tukaimarisha misingi ya utaifa wetu ambayo ni uzalendo, amani, umoja, upendo, mshikamano, kuvumiliana na kusameheana.

Ninatoa shukrani zangu za pekee kwa viongozi wa dini zote, na waumini wa dini zote, kwa jinsi tulivyoshirikiana vizuri sana katika msiba huu wa kitaifa. Natoa shukrani kwa viongozi na wanachama wa vyama vyote vya siasa. Maana tumeshirikiana vizuri sana; kwenye msiba huu, tofauti zetu za kisiasa hazikuonekana. Ninawashukuruni sana. Na hii ndiyo asili na heshima yetu Watanzania mbele ya mataifa mengine. Tumuenzi ndugu yetu, na ndugu yetu sote, Dr. Omar Ali Juma, kwa kuendeleza sifa hizo. Hasa hapa Pemba ambapo ni nyumbani kwake, na ambapo nia na makusudio yake siku zote yalikuwa kurejesha upendo, mshikamano, furaha na amani, hata pale tunapopingana kisiasa, na kuharakisha maendeleo ya watu wa Pemba na Tanzania nzima, kwa manufaa na maslahi ya jamii nzima.

Tumkumbuke Dr. Omar Ali Juma pia kwa kuongeza kasi katika vita dhidi ya umaskini na uharibifu wa mazingira. Maana kati ya mambo yaliyomkera sana, na akapania kuongoza vita dhidi yake, ilikuwa ni umaskini, na pacha wake ambaye ni uharibifu wa mazingira, mama yao akiwa ni ujinga – kama ambavyo Mzee Mwinyi amewahi kutuasa.

Dr. Omar Ali Juma alikuwa msaidizi wangu hodari sana na mwadilifu kwenye eneo hili la umaskini, mazingira na elimu; na akapeleka ujumbe huo kila pembe ya nchi yetu ya Tanzania, kwa watu wote, wa kabila zote na dini zote. Maana sote tunastahili mafanikio na manufaa sawa ya maendeleo, utunzaji wa mazingira na kupata elimu. Naomba tumuenzi kwa sote kuendeleza vita hivyo.

Dr. Omar Ali Juma alipenda umoja, akachukia utengano. Alikuwa Mtanzania kweli kweli, aliyetetea na kuimarisha Muungano wetu, na siku zote kuchangia mawazo mazuri juu ya namna bora ya kunoa utendaji wa Serikali zake na taasisi zake zote kwa faida ya pande zote na watu wote. Kazi yake hiyo lazima tuindeleze kwa bidii zaidi.

Ninaishukuru kamati iliyoandaa mazishi haya, na wote walioshiriki katika maandalizi yote yaliyotuwezesha kumweka mwenzetu mahali pake pa kupumzika kwa heshima zote alizostahili. Kwa njia ya pekee nawashukuru sana wanajeshi wetu, kwa kazi yao nzuri, kama ilivyo kawaida yao.

Ninashukuru sana kwa fursa niliyopata ya kufanya kazi kwa karibu sana na marehemu wetu, Dr. Omar Ali Juma. Ninamwomba Mwenyenzi Mungu ampe mjane wake, watoto wake, ndugu zake na Watanzania wote, moyo wa utulivu, upendo, amani na matumaini katika kipindi hiki kigumu sana.

Katika siku hii ya majonzi makubwa, nakumbuka maneno ya mwana-falsafa mmoja aliyeishi karne mbili zilizopita akisema:
"Maisha ni mafupi, na hatuna muda mwingi sana wa kufurahisha nyoyo za wale tunaosafiri nao katika dunia hii yenye kiza. Uwe mwepesi basi wa kupenda! Ufanye haraka kuwa mwema kwa mwenzako!"

Dr. Omar Ali Juma alisafiri nasi katika dunia hii ya kiza, ya taabu nyingi. Lakini alifurahihisha nyoyo zetu kwa kuwa mwepesi wa upendo na wema.

Tumwombe Mwenyenzi Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi.

Mungu Ibariki Tanzania.
Mungu Ibariki Afrika.

No comments:

Post a Comment