Tuesday, January 3, 2012

Maisha ya awali

Dk. Omar alizaliwa tarehe 26 Juni, 1941 katika kijiji cha Wawi, Wilaya ya Chakechake, Kusini mwa Mkoa wa Pemba.
Elimu yake ya msingi aliipata katika Shule ya Msingi ya wavulana ya Chake, ambayo kwa sasa inajulikana kama Shule ya Msingi Michakaini tangu mwaka 1949 mpaka mwaka 1957.
Elimu ya sekondari aliipata katika Shule ya Sekondari ya Euan Smith Madressa, ambayo nayo hivi sasa imebadilishwa jina na kuitwa Shule ya Sekondari ya Haile Selassie tangu mwaka 1957 hadi 1960. Kuhusu elimu ya juu aliipatia kwenye vyuo mbalimbali tofauti vilivyomo nchini Tanzania na nje.
Alianza kusoma katika Chuo Kikuu cha Moscow State, ambako alimaliza mwaka 1967 na pia mwaka 1969 alimaliza katika Chuo Kikuu cha Cairo, Misri.
Pia alisoma Chuo Kikuu cha Edimburgh ambapo napo alimaliza masomo yake mwaka 1977, akapata nafasi tena ya kwenda kusoma Chuo Kikuu cha Florida, Marekani na alimaliza mwaka 1980.
Dk. Omar aliendelea na masomo yake na mwaka 1982 alikuwa mmoja wa wahitimu katika Chuo Kikuu cha Reading, Uingereza na pia kiongozi huyu alipata fursa ya kwenda kusoma katika Chuo cha Kivukoni Ideological mwaka 1982.

Shughili za Kiserikali

Dk. Omar Ali Juma alikuwa mfanyakazi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tangu mwaka 1967 hadi mwaka 1984 ambapo alihamishiwa katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1995 hadi alipofariki dunia.
Alipokuwa mfanyakazi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) alishika nyadhifa nyingi kubwa.
Mwaka 1967 - 1969 alikuwa Ofisa Wanyama Msaidizi, mwaka 1969 - 1970 alikuwa Ofisa Wanyama na mwaka 1970 hadi 1971 alikuwa Ofisa Wanyama Mwandamizi.
Mwaka 1971 -1972 alikuwa Ofisa Mifugo, pia alikuwa Ofisa Mkuu wa Mifugo katika miaka ya 1972-1978.
Wakati mwaka 1978-1984, alifanikiwa kushika wadhifa wa Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mifugo, mwaka 1984-1987 alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Maendeleo ya Mifugo, Zanzibar, na Januari 1988 - 1995, alikuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

 

No comments:

Post a Comment